MAJALIWA , HAKUNA MGONJWA ATAKAYEKOSA DAWA.
Na John Richard
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga fedha nyingi
kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba na kwamba hakuna mgonjwa
atakayekwenda kutibiwa katika hospitali, vituo vya afya au zahanati bila
ya kupatiwa dawa.
Ameyasema hayo jana jioni (Jumatatu, Julai 10, 2017), wakati akizungumza
na wananchi wa wilaya ya Liwale katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
Uwanja wa Michezo wa Wilaya.
Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa katika ziara
yake ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi, alisema Serikali haitaki kusikia
wananchi wanakwenda hospitali, Vituo vya afya au zahanati na kukosa dawa.
Alisema moja kati ya ajenda muhimu ya Serikali ya awamu ya Tano ni
kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake, ambapo kila mwezi halmashauri zote
nchini zinapelekewa fedha za ununuzi wa dawa.
“Serikali hii ya Rais Dkt. John Magufuli inatoa fedha za kununulia dawa
kila mwezi katika halmashauri zote nchini. Sasa kama hapa Liwale kuna
malalamiko ya wananchi kukosa dawa katika hospitali yetu, Mkuu wa Wilaya
kafuatilie huko Halmashauri ili kujua wanapeleka wapi fedha za dawa.”
Katika bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto ya mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi bilioni 236 zimetengwa
kwenye ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi alisema hali ya
upatikanaji wa dawa muhimu kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 iliongezeka kwa
asilimia 50 ikilinganishwa na ile ya mwaka 2015/2016.
Bw. Zambi alisema katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka 2016 hadi
Februari 2017 mkoa wa Lindi ulipokea sh milioni 538 kwa ajili ya ununuzi wa
dawa kupitia Bohari ya Dawa (MSD).
“Hospitali ya mkoa ilipokea sh. milioni 195,328,186 kwa ajili ya
ununuzi wa dawa na pia ilitumia sh. Milioni 127,171,700 toka fedha za
uchangiaji kwa ununuzi wa dawa.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji wa
Halmashauri kwenda vijijini na kuwaelimisha wananchi umuhimu wa utunzaji wa
mazingira ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
Pia amewaagiza Maofisa Kilimo wote kuhakikisha wanaacha kushinda
maofisini na badala yake waende mashambani kwa ajili ya kuwaelimisha wakulima
namna bora ya kulima kwa kufuata njia za kisasa ili kupata tija.
No comments