Header Ads 728*90

WAZIRI LWENGE AKUTANA NA WAZIRI WA MAJI WA MISRI



Na John richard
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge amekutana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Misri, Dkt. Mohamed Abdel Aty kwa mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali za Tanzania na Misri katika utekelezaji wa miradi ya Sekta za Maji na Umwagiliaji.

Kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi za Wizara za Dar es Salaam kilihusisha mazungumzo ya utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano wa mataifa ya Misri na Tanzania, hususani katika utekelezaji wa miradi ya majisafi na kilimo cha umwagiliaji nchini kwa serikali hizo mbili.
Katika kikao hicho Inj. Lwenge alisema Tanzania na Misri ni mataifa yanayoshirikiana katika sekta mbalimbali, na kupitia ushirikiano huo lengo kubwa ni kuinua Sekta za Maji na Umwagiliaji.

“Kwa msaada wa Serikali ya Misri, serikali imefanikiwa kutekeleza mradi wa maji wa visima 30 kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya majisafi kwa wilaya kame za Same, Mwanga, Kiteto, Bariadi na Itilima kwa awamu ya kwanza na bado wapo katika mazungumzo ya kutekeleza miradi mingine mingi”, alisema Waziri Lwenge.

“Lakini pia tuna lengo la kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, kwa kutumia teknolojia ya kisasa yenye kutumia maji kidogo na kuzalisha chakula kingi. Hivyo, kwa kushirikiana na wenzetu wa Misri wenye utaalamu wa hali ya juu, tunataka kufanikisha jambo hilo ili tuhakikishe usalama wa chakula na chakula kutosha kwa ajili ya wananchi”.

Inj. Lwenge alisema ushirikiano baina ya Serikali za Tanzania na Misri utaleta tija kwa Tanzania, hasa ikizingatiwa taifa hilo limepiga hatua kubwa katika Sekta za Maji na Umwagiliaji na kwa kubadilishana uzoefu, kutaisaidia Tanzania kupiga hatua kubwa katika sekta hizi muhimu kwa taifa katika kutizima azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania kuwa Nchi ya Viwanda.

Naye, Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Misri, Dkt. Mohamed Abdel Aty alisema wataendelea kudumisha uhusiano wake na  Tanzania kwa kuchangia maendeleo ya Tanzania kupitia ushirikiano kwenye sekta za maji, umwagiliaji na hata usafirishaji utakaoleta tija kubwa kwa ustawi wa mataifa haya.


Dkt. Abdel Aty aliambatana na ujumbe uliojumuisha Balozi wa Misri nchini Tanzania Yasser Ahmed Al Eldin Elshawaf, Mwenyekiti wa Sekta ya Maji ya Nile, Ahmed Bahaa Eldin Mohamed na Kansela wa Ubalozi wa Misri nchini Tanzania, Moataz Kareem, huku ujumbe wa Inj. Lwenge ukijumuisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo, Mkurugenzi Msaidizi wa Majishirikishi, Sylivester Matemu, Mkurugenzi Msaidizi Mipango na Utafiti, Dkt. George Lugomela na Mkuu wa Kitengo cha Sheria, Simon Nkanyemka.
Aidha, Waziri Lwenge alimpeleka mgeni wake, Waziri Abdel Aty kutembelea Maonesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa – Sabasaba, kwa nia ya kumuonyesha maendeleo ya Sekta ya Biashara nchini, yaliyovutia kampuni 25 kutoka Misri na kushiriki katika maonesho hayo.


No comments

Powered by Blogger.