Header Ads 728*90

NYAMBIZI YA MAREKANI YATIANANGA KOREA KUSINI


NYAMBIZI ya jeshi la Marekani imewasili katika pwani ya Korea Kusini huku wasiwasi ukiongezeka kuhusu uwezekano wa Korea Kaskazini kufanya jaribio jingine la kombora au silaha za nyuklia.
Meli hiyo kwa jina USS Michigan, ambayo ina uwezo wa kushambulia kwa makombora, inatarajiwa kujiunga na kundi jingine la meli za kivita zinazoelekea eneo hilo, zikiongozwa na meli kubwa ya kubeba ndege ya Carl Vinson.
Korea Kaskazini inaadhimisha miaka 85 tangu kuanzishwa kwa jeshi lake Jumanne.
Miaka ya nyuma, imekuwa ikiadhimisha siku hiyo kwa kuzindua makombora na silaha nyingine.
Wasiwasi umeongezeka wiki za karibuni kutokana na Marekani na Korea Kaskazini kujibizana vikali na kutoleana vitisho.
Hayo yakijiri, katika tukio ambalo si la kawaida, bunge lote la Seneti nchini Marekani limealikwa kwa kikao cha kupashwa habari kuhusu Korea Kaskazini siku ya Jumatano katika ikulu ya White House.
Nyambizi ya USS Michigan hutumia nguvu za nyuklia na hubeba makombora aina ya 154 Tomahawk na wanajeshi 60 pamoja na meli nyambizi nyingine ndogo, gazeti la Korea Kusini la Chosun Ilbo limeripoti.
Meli hiyo inatarajiwa kushiriki kwenye mazoezi ya kijeshi pamoja na kundi la meli zinazoongozwa na Carl Vinson, kundi ambalo lilitumwa eneo la Korea kuonyesha ubabe wa kijeshi wa Marekani.
Meli hizo za kivita wakati mmoja zilizua utata baada ya suitafahamu kuhusu iwapo zilikuwa hasa zinaenelekea eneo la Korea.
Lakini maafisa wa jeshi la wanamaji la Marekani kwa sasa wamesema zinaelekea eneo hilo kama ilivyoamrishwa.
USS Carl Vinson mwanzoni ilikamilisha mazoezi na jeshi la Australia na kisha kuondoka ikidhaniwa kwamba ilikuwa inaelekea pwani ya Korea.
Lakini meli hiyo na meli nyingine zilipita na kuelekea upande wa Bahari ya Hindi.

No comments

Powered by Blogger.